Alhamisi 9 Oktoba 2025 - 14:47
Zitumike mbinu za kisasa na vitu vyenye ushawishi katika kufundisha na kueneza swala

Hawza/ Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, katika ujumbe wake kwenye Mkutano wa 32 wa Kitaifa unaohusiana na Swala, amesisitiza kuwa taasisi zinazoeneza dini, viongozi wa dini, na waumini wote, wanapaswa kuzingatia jambo hili kama jukumu lisiloepukika; na kutumia mbinu za kisasa na njia zinazovutia kwa ajili ya kufundisha swala, kueneza ibada hiyo, kubainisha undani na uzuri wa maana yake, na hatimaye kueleza umuhimu wa swala kwenye maisha ya kila Muislamu duniani na Akhera.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei katika ujumbe wake kwa ajili ya kikao cha 32 cha Kitaifa kinacho husiana na Swala, akibainisha nafasi ya faradhi hii iliyojaa maana na sehemu ya uhai wa mwanadamu duniani na Akhera, amesisitiza kuwa:


“Kuieneza na kuifundisha swala, kubainisha undani wa kiroho wa swala na kushikamana nayo, ni jukumu la lazima la taasisi za kueneza dini, viongozi wa dini na waumini, ambao wanapaswa kutumia mbinu za kisasa katika mwelekeo huu.”

Matni kamili ya ujumbe wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ni kama ifuatavyo:

بِسْمِ اللهِ الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ
Na rehema na amani zimshukie Muhammad na Ahlul-Bayt wake watoharifu

“Kikao kwa ajili ya Swala ni moja ya vikao vyenye manufaa makubwa zaidi, na siku ambayo kikao hiki kinafanyika ni miongoni mwa siku zilizo na baraka zaidi katika mwaka. Hii ni kwa sababu ya upekee na umuhimu wa faradhi hii yenye maana kubwa na sehemu ya maisha, miongoni mwa faradhi zote za Kiislamu.

Swala, inapotekelezwa kwa kufuata adabu zake kama vile unyenyekevu na kujitoa kwa Mola, huleta utulivu moyoni, huimarisha azma, huifanya imani iwe ya kina na kuhuisha matumaini. Hatima ya mwanadamu duniani na Akhera inautegemea moyo kama huo, azma kama hiyo, imani kama hiyo na matumaini kama hayo. Ndio maana katika Qur’ani na maandiko mengine ya dini, wosia kuhusiana na swala ni zaidi kuliko usia mwengine wowote; na ndio maana katika adhana, swala hutangazwa kuwa ni bora kuliko shughuli zote nyingine.

Wazazi, walimu, marafiki na wenye kuandamana nao, na vile vile taratibu na ada za kimaisha zinzohusiana na swala, vyote hivi vina nafasi muhimu katika kuieneza na kushikamana nayo.

Taasisi za kueneza dini, viongozi wa dini, pamoja na waumini wote, wanapaswa kuzingatia jambo hili kama jukumu lisiloepukika, na kutumia mbinu za kisasa na njia zenye kuvutia kwa ajili ya kufundisha swala, kueneza swala, kubainisha undani wake wenye maana kubwa, na pia kuonesha haja ya kila Muislamu kwenye swala ndani ya maisha yake duniani na Akhera.

Ni wajibu wangu pia kutoa shukrani za dhati kwa Ustadh Qaraati, ambaye ameotesha mti huu wenye matunda mengi na kuuendeleza hadi kufikia hatua hii.”

وَالسَّلامُ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَةُ اللهِ
Sayyid Ali Khamenei

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha